Friday, November 27, 2015

WAZIRI MKUU AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA TRA

Waziri Mkuu Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa leo ameamuru kukamatwa kwa maafisa kadhaa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na wengine kufukuzwa kazi baada ya kufanya ziara ya kushtukiza Bandarini na kukuta madudu ambayo hakuyafurahia.

Maafisa hao, ambao kwa sasa tunahifadhi majina ili Jeshi la Polisi liweze kuwashughulikia, wametakiwa pia kusalimisha hati zao za usafiri.

Hii imekuja baada ya kugundulika kwamba kuna makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 80 ambayo data za Mamlaka ya Bandari inazo lakini katika mtandao wa TRA hayaonekani.
Majaliwa Kassim Majaliwa  akimkabidhi Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade orodha ya makontena  349. yenye kodi ya serikali ya thamani ya  shilingi bilioni 800 yalitoka kwenye bandari ya Dar es salaam bila kulipiwa kodi.
Waziri Mkuu Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa akimwonyesha orodha ya makontena 349 yaliyopotea yenye thamani ya shilingi bilioni 80 na TRA haina taarifa.
Waziri Mkuu Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa akiagana na viongozi wa TRA na TPA.

WAZIRI MKUU AWABANA UPOTEVU WA MAKONTENA 349, YENYE THAMANI YA TSH. BILIONI 80/=

WAZIRI MKUU Majaliwa Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi maafisa watano na watumishi watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana na upotevu wa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 80/-.
Akizungumza na viongozi wa Mamlaka ya Bandari pamoja na viongozi wa TRA katika ziara ya kushtukiza leo mchana (Ijumaa, Novemba 27, 2015), Waziri Mkuu amewataka Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Rished Bade na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Lusekelo Mwaseba wahahakikishe wanashirikiana na polisi kufuatilia upotevu huo na kwamba fedha hizo zinapatikana na zinarudi Serikalini.

Akitangaza uamuzi huo baada ya kufanya kikao na baadhi ya viongozi wa Serikali bandarini hapo, Waziri Mkuu aliwataja maafisa waliosimamishwa kazi kuwa ni Kamishna wa Forodha, Bw. Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Bw. Habibu Mponezya.

“Hawa wanasimamishwa kazi. IGP ninaagiza hawa watu wakamatwe na kuisaidia polisi. Hati zao za kusafiria zikamatwe na mali zao zikaguliwe kama zinaendana na utumishi wa umma,” alisema Waziri Mkuu.

Maafisa wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa kitengo cha TEHAMA, Bw. Haruni Mpande, Bw. Hamisi Ali Omari (hakutaja ni wa idara gani), na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD In-Charge), Bw. Eliachi Mrema. “Hawa wanasimamishwa kazi hadi uchunguzi utakapokamilika na pia wawe mikononi mwa polisi,” alisema.

Pia aliagiza watumishi watatu wa mamlaka hiyo wahamishwe kutoka Dar es Salaam na kupelekwa mikoani. Watumishi hao ni Bw. Anangisye Mtafya, Bw. Nsajigwa Mwandengele na Bw. Robert Nyoni.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwagiza Katibu Mkuu wa Hazina, Dk. Servacius Likwelile ambaye alikuwepo kwenye kikao hicho, kuhakikisha kuwa anapeleka wataalamu kutoka Wakala wa Serikali Mtandao (e-Govt) haraka iwezekanavyo ili wakakague mifumo ya taarifa na kubaini jinsi ambavyo wizi huo unafanyika.

“Ninataka uchunguzi uanze kufanyika mara moja, tafuteni njia ambazo zinatumika kama mianya ya wizi kutokea hapa bandarini hadi kwenye ICDs. Nataka hayo makontena yatafutwe hadi yajulikane yako wapi, na fedha hiyo ihakikishwe inarudi serikalini,” alisema.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Bw. Ernest Mangu, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Florens Turuka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dkt. Shaaban Mwinjaka, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya DSM, Suleiman Kova, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Bw. Awadh Massawe na viongozi mbalimbali kutoka TRA na TPA.

Mapema akijibu maswali ya Waziri Mkuu, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Bade alikiri kwamba kuna upotevu wa makontena ambao huwa unafanyika kati ya bandarini na ICDs na hasa ICD ya Ubungo. Akitoa ufafanuzi, alisema kwamba walifanya ukaguzi kwenye ICD moja na kukuta makontena 54 yamepotea kwa njia za wizi.

“Hata hivyo, tulipoendelea na ukaguzi, namba iliongezeka na kufikia 327. Tunaendelea kufuatilia kwa kushirikiana na TAKUKURU. Mmiliki wa ICD ametakiwa kulipa faini sh. bilioni 12.6/- na ameshalipa sh. bilioni 2.4/-,” alifafanua.

Alipoulizwa na Waziri Mkuu kama ana majina ya watumishi wanaohusika na wizi huo, Bw. Bade akakiri kwamba anayo lakini siyo kwa wakati huo labda ayapate kutoka kwa wasaidizi wake. Ndipo Waziri Mkuu akamuonyesha orodha ya makontena 349 yenye taarifa zote hadi namba za magari yaliyobeba mizigo hiyo na Bw. Bade akakiri kwamba orodha hiyo ni ya kweli.

“Kwa utaratibu huo hatuwezi kufika, labda baadhi ya watu waondolewe kazini”. Ndipo akaanza kutaja majina ya maafisa hao waliosimamishwa kazi.



IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
IJUMAA, NOVEMBA 27, 2015.


Wednesday, November 25, 2015

JUKWAA HURU LA WAZALENDO KWA RAIS DK. JOHN MAGUFULI.


Mwenyekiti wa Jukwaa Ally Salum akizungumza na Waandishi wa habari leo katika hoteli ya Travertine, Magomeni jijini Dar es Salaam (kulia)  Katibu wake, Mtela Mwampamba.

JUKWAA HURU LA WAZALENDO

TAMKO LA JUKWAA KWA VYOMBO VYA HABARI
 
Ndugu Wanahabari,

Mbele yenu sisi tuliowaita hapa ni Jukwaa Huru la Wazalendo ambalo limeitisha mkutano huu ili kufikisha yale tuliyoyakusudia kuwaeleza umma wa watanzania.

Sote tunatambua kuwa nchi yetu imetoka katika uchaguzi mkuu ambao umetupatia viongozi wapya wa awamu ya tano ya uongozi wa taifa letu chini ya Dr. John Pombe Joseph Magufuli. Tunapenda kuwapongeza watanzania wote kwa uchaguzi wa amani na utulivu. Aidha kwakua ndio mara yetu ya kwanza kuzungumza nanyi tunapenda kuwapongeza wanahabari wote kwa kazi nzuri ambayo mmekua mkiifanya kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu nchini. Tunawashukuru sana.

Mkutano wetu huu umebeba madhumuni makubwa mawili.
Kwanza ni kumpongeza Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba yake aliyoitoa Bungeni siku ya ufunguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 19/11/2015. Tunaiunga mkono Hotuba yake ambayo kwa kweli ilikuwa imebeba Uzalendo, Ujasiri, dira ya kweli ya maendeleo ya taifa letu na muuelekeo mpya wa Serikali ya awamu ya tano. Mambo yote aliyozungumzia Mh. Rais yamebeba maslahi mapana ya nchi yetu na yanalenga kuijenga Tanzania mpya ambayo waasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume walikusudia kuijenga.

Pili, pamoja na mambo mengi yaliyogusiwa na hotuba ya Mh. Rais, eneo la kubana matumizi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa Serikali ni moja katika mambo ambayo Jukwaa hili limeamua kuyaunga mkono kwa vitendo. Mh. Rais alitoa mchanganuo wa eneo moja tu la safari za nje na jinsi lilivyo ligharimu Taifa mabilioni ya shilingi na kuahidi kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wake itajikita katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

Aidha Mh. Rais ameanza kutekeleza kwa vitendo ahadi yake hiyo ya kupunguza matumizi yote yasiyo ya lazima Serikalini, ikiwemo hafla, warsha, makongamano na safari za nje.

Jukwaa Huru la Wazalendo, linatambua kuwa kwa miaka kadhaa mbunge wa Kigoma Mjini Mh. Zitto Kabwe amekuwa na msimamo wa kutokupokea posho za kitako tangu akiwa mbunge wa Kigoma Kaskazini katika Bunge la 10. Pamoja na Mh. Zitto, Jukwaa pia limepokea taarifa za baadhi ya wabunge wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walioamua kuunga mkono juhudi za Mh. Rais za kupunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini kwa kukataa hadharani kupokea posho ya kitako ya mbunge
(sitting allowance).

Mnamo tarehe 23/11/2015, mbunge wa Singida Magharibi (CCM) Mh. Elibariki Imanuel Kingu alimwandikia barua Katibu wa Bunge akieleza msimamo wake wa kukataa kulipwa posho ya kitako ya Bunge (sitting allowance) katika kipindi chote cha miaka mitano (2015 - 2020). Huyu anakuwa ni mbunge wa pili baada ya Mh. Zitto Kabwe kutoka hadharani na kukataa posho ambazo msingi wake ni unyonyaji wa wanyonge na ubadhirifu wa kodi za wananchi.

Jukwaa linapenda kumpongeza Mh. Kingu Mbunge kwa ujasiri wake na Uzalendo kwa Taifa lake, uliomfanya kuunga mkono juhudi za Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vitendo.
Jukwaa linatambua ya kwamba, mapambano ambayo Mh. Kingu Mbunge ameyaanzisha ni makubwa, magumu na yanahitaji kuungwa mkono na watanzania wote wanaoipenda nchi yao bila kujali itikadi za vyama. Tunafahamu, wapo baadhi ya wabunge wabinafsi na wasio na huruma na wanyonge wa Taifa letu ambao hawajafurahishwa na hatua hii ya wabunge kama Zitto na Kingu ya kukataa posho ya kitako. Baadhi ya wabunge wameanza kumpigia simu na kumtumia jumbe (sms) za vitisho mh. Elibariki Kingu (MB) na wengine wakibeza kuwa anatafuta cheo.

Jukwaa linalaani hatua za wabunge hao wanaopinga nia njema ya Mh. Elibariki Kingu na Mh. Zitto Kabwe kwa uamuzi wao wa kukataa posho za kinyonyaji na hivyo basi, Jukwaa linawaomba wananchi wote majimboni, kuwataka wabunge wao waliowachagua kueleza misimamo yao hadharani juu ya kuunga mkono hatua ya kukataa posho kama njia ya kupunguza matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima.

Jukwaa linafahamu ya kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kuidhinisha masharti ya kazi za kibunge na stahiki wanazopaswa kulipwa katika kazi hiyo.

Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, tunamuomba na kumshauri Mh. Rais John Pombe Magufuli atakapokuwa anaidhinisha masharti na stahiki hizo, atusaidie kuifuta kabisa posho ya kitako ya wabunge (sitting allowance).

Aidha, Jukwaa linamuomba mh. Rais kuzipitia na kutoa agizo la kufutwa kwa posho zote zisizo za lazima zinazolipwa kwa watumishi wa umma wa kada mbalimbali yakiwemo mashirika ya umma.

Jukwaa letu linatoa wito kwa wabunge wote bila kujali vyama vyao, kuungana na Mh. Kingu(MB) na Mh. Zitto(MB) katika kukataa malipo ya posho ya kitako ili kupunguza mzigo mkubwa ambao Serikali inaubeba kuhudumia wabunge. Fedha hizi ni vyema zielekezwe katika kutatua kero za wananchi vijijini kama vile ukosefu wa maji, madawati, vitanda vya Hospitali n.k.

Tunasisitiza kwamba, Ubunge ni Utumishi,na wala sio Utukufu. Kazi ya Mbunge ni kuwawakilisha wananchi wake na si kuwanyonya. Tufike mahali kama Taifa tuwe na nidhamu ya matumizi ya kodi za wananchi na mgawanyo sawa wa keki ya Taifa. Kuendelea kulipana posho hizo ni ishara ya unyonyaji, dhuluma na kuongeza pengo kati ya wenye nacho na wasionacho nchini. Jambo hili linakuza chuki na hasira miongoni mwa wananchi wa hali ya kawaida dhidi ya viongozi wao na serikali kwa ujumla.

Tunawaahidi kuwa Jukwaa litaendeleza harakati (movement) na vuguvugu hili kwa kuanzia na Bunge kwasababu ndio wawakilishi wa wananchi. Tutaendelea kupaza sauti zetu ili wabunge wengi zaidi Wazalendo wajitokeze na kukataaa posho hizi. Tunajua kuwa wapo miongoni mwao wabunge wazalendo ambao wataguswa na wito huu na kuuunga mkono hadharani.

Aidha tutaendelea kuwasemea kwa wananchi wabunge ambao bado hawataki kukataa posho hizi bila kujali vyama vyao. Tunawaomba wananchi kote nchini kutuunga mkono katika harakati hizi ili tuweze kuokoa mabilioni ya shilingi yanayopotea kila Bunge linapokaa Dodoma kupitia posho ya kitako (sitting allowance).
Ahsanteni sana.

ALLY SALUM HAPI - MWENYEKITI (0714 193161
MTELA MWAMPAMBA - KATIBU (0755 178927)


Tuesday, November 24, 2015

MCHUJO WA DARASA LA PILI KUPITIA NECTA

BARAZA la Taifa la Mitihani (NECTA) limesema ili kutekeleza sera ya elimu ya mwaka 2014, watoto wataanza kukariri darasa kuanzia wakiwa darasa la pili.

Alisema hatua hiyo itachukuliwa endapo watashindwa mtihani wa kujipima ambao utaanza rasmi mwakani kwa wanafunzi wa ngazi hiyo ya elimu.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipozungumza na gazeti hili.

Alisema kufanyika kwa mitihani hiyo kunakwenda sambamba na kuipa hadhi mitihani ya kupima wanafunzi katikati ya masomo ya darasa la nne na kidato cha pili ambayo kwa sasa itakuwa chini ya baraza hilo tofauti na ilivyokuwa awali.

Dk. Msonde alisema kwa upande wa mitihani ya darasa la pili, matokeo ya mitihani hiyo itasaidia kuwatenga wanafunzi hao kwenye makundi matatu ambayo walimu watatakiwa kuyafanyia kazi kuhakikisha watoto hao wakiendelea na madarasa ya juu watafanya vizuri.

Alisema kwa kuwaandaa watoto kwa mitihani hiyo, anaamini mpaka wakiwa wanamaliza darasa la saba hakuna ambaye atakuwa hajapata stadi za kusoma na kuandika kama ilivyo kwa sasa ambako baadhi uhitimu elimu ya msingi wakiwa hawajui kusoma na kuandika.

“Kwa kuanza kuwapima wakiwa darasa la pili watakuwa wanaangalia kwenye stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu huku mitihani mingine kama ile ya darasa la nne ikipandishwa hadhi na kuwa chini ya baraza.

“Tunaamini suala la watoo kumaliza darasa la saba baadhi wakiwa hawajui kusoma na kuandika litaisha,” alisema.

Alisema mipango ya sera hiyo ikikamilika, mtihani wa darasa la saba ambao hivi sasa ni wa kuhitimu elimu ya msingi, utakuwa wa kupima kama ulivyo ule wa darasa la nne kwa sababu elimu ya msingi mwisho itakuwa kidato cha nne.

“Siwezi kusema ni lini hili litaanza kwa sababu utekelezaji wa sera ni mchakato, lazima kwanza madarasa ya sekondari yaongezwe.

“Mitaala ibadilike kama hivi sasa ambavyo ya darasa la kwanza na la pili imebadilika na ndiyo kwanza tunaanza kuwapima wanafunzi kwa mtihani huo wa darasa la pili.

“Faida nyingine ya mtihani huo na ule wa darasa la nne ni kuhakikisha mpaka mtoto anafika darasa la saba, wale watakaopata alama 100 chini ya 250 ambao kwa sasa ndiyo ufaulu wawe wameongezeka,” alisema Dk. Msonde.

Alisema ili kuona namna bora ya kuanza kufanya mtihani huo mwakani, leo watoto wa darasa la pili kutoka shule 66 zilizo kwenye mikoa 11 watafanya mtihani huo ikiwa ni sehemu ya majaribio.

Alisema kwenye mikoa hiyo zimechaguliwa wilaya ambazo zimetoa shule moja ya kijijini, moja ya mjini na nyingine ya mchepuo wa Kiingereza.

Sunday, November 22, 2015

MH. JOHN MAGUFULI BAADA YA KULIZINDUA BUNGE.


Mh. John Pombe Magufuli  wakibadilishana mawazo na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi  baada ya kulihutubia Bunge la kumi na moja (11) na kulizindua Mjini Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. John Pombe Magufuli (Kushoto)  Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, (Kulia) Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, baada ya kuhutubia Bunge la 11, Mjini Dodoma.
Mh,Dk. John Magufuli akimkabidhi cheti Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB Mama Ineke Bussemaker kwa mchango wao.

Mh. John Pombe Magufuli akimshukuru na kumkabidhi cheti mwakilishi wa Benki kwa mchango wao baada ya kulizindua rasmi Bunge la 11 Mjini Dodoma.

Friday, November 20, 2015

UZINDUZI RASMI WA BUNGE LA KUMI NA MOJA (11).


Mh,Dkt. John Pombe Joseph Magufuli rais wa Jamhuli ya Muungano wa Tanzania amelihutubia bunge kwa mara ya kwanza inchini, akisisitiza kuwa Bunge ni chombo muhimu, halipaswi kuwa chombo cha malumbano, kutukanana, kutoka nje, n.k. Katika hotuba ya Mh.Rais John Pombe Joseph Magufuli Amesema anachukizwa sana na vitendo vya rushwa na ufisadi, Pia kasisitiza kuwa atahakikisha safari zote za nje ya nchi zinadhibitiwa ili kuongeza mapato ya nchi.

HOTUBA YA MHESHIMIWA DK. JOHN POMBE MAGUFULI.

Thursday, November 19, 2015

KUAPISHWA KWA WAZIRI MKUU KATIKA VIWANJA VYA IKULU.

Mh.John Pombe Magufuli akimkabidhi hati ya kiapo Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Kassim baada ya uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Joseph Magufuli  katika picha na Makamo wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan (Kulia) Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Kassim.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Magufuli katika picha ya pamoja na familia ya Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Kassim baada ya kuapishwa katika viwanja vya Ikulu Dodoma.

DK. TULIA ACKSON NAIBU SPIKA WA BUNGE LA TANZANIA.

Dk.Ackson Mwansasu Naibu Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akila kiapo baada ya kuchaguliwa na Wabunge Mjini Dodoma.



Thursday, November 5, 2015

RAIS DK. JOHN POMBE MAGUFULI AKIELEKEA IKULU.

Rais Dk. John Pombe Magufuli  akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli akiwasili Ikulu mara baada ya Kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mh. Dk Ally Mohamed Shein rais wa Zanzibar wakibadilishana mawazo na  Uhuru Kenyata wakati wa hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mke wa Raila Odinga, na Mama Janeth Magufuli akisalimiana na Raila Odinga katika Picha.
Dk.John Pombe Magufuli rais wa Jamhuri wa Mungano wa Tanzania katika picha ya Pamoja.

Posted By Emman W

KUAPISHWA KWA RAIS DR.JOHN MAGUFULI

Rais wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania Mh, Dk. John Pombe Magufuli akiwashukuru watanzania wote kwa kumchagua kuwa rais wa awamu ya tano, pia kawataka viongozi wa upinzani kushirikiana na serikali yake.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh, Dk. John Pombe Magufuri akisalimiana na Rais wa Zanzibar Dokta Ali Mohammed Shein katika Jukwaa la uwanja wa Taifa (Uhuru).

Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. JOHN POMBE MAGUFULI akila kiapo katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, ''Mimi John Pombe Magufuli naapa nitatenda kazi zangu za urais kwa mujibu wa sheria na mila na desturi za Jamhuri ya muungano wa Tanzania, ewe mwenyezi mungu nisaidie Amen.''  



Makamu wa rais wa Kwanza mwanamke nchini Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan akiweka sahii ya kiapo katika Uwanja wa Taifa Jijin Dar es Salaam.


Posted By Emman



SHEREHE ZA KUAPISHWA KWA RAIS WA AWAMU YA TANO.

Umati wa watu katika Jukwaa la Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam wakisherekea kuapishwa kwa Dk. John Pombe Magufuli.








Wednesday, November 4, 2015

MAANDALIZI YA UWANJA WA UHURU DAR ES SALAAM



Maandalizi ya Kuapishwa Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli katika Uwanja wa Uhuru Jijin Dar Es Salaam