Saturday, December 12, 2015

KUAPISHWA KWA BARAZA LA MAWAZIRI NA HM. MAGUFULI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli akimuapisha Ummy Ally Mwalimu kuwa Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.
Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akimuapisha Mh. Nape Nnauye kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo Ikulu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akimuapisha Jenista Joakim Mhagama kuwa Waziri wa Nchi , Ofisi ya Waziri Mkuu Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Dk. Abdallah Saleh Possi kuwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye ulemavu) Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mh, Rais Dk. John Pombe Magufuli akimuapisha Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akimkabidhi  Muongozo wa kufanyia kazi  kwa Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Harrison George  Mwakyembe mara baada ya kumuapisha Ikulu jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akimuapisha Profesa Sospeter Mwijarubi Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dk. John Pombe Magufuli katika picha ya pamoja na Mawaziri wake mara baada ya kuwaapisha Jijini Ikulu Dar es salaam.

Thursday, December 10, 2015

MHE.RAIS JOHN MAGUFULI ATANGAZA BARAZA LA MAWAZIRI



Rais John Magufuli akitangaza baraza la mawaziri Ikulu jijini Dar es salaam, Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na kushoto ni Waziri Mkuu Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa.

BARAZA LA MAWAZIRI TANZANIA

Wizara ya Ofisi ya Rais,Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora.
  • Mawaziri - George Simbachakene na Angella Kairuki
  • Naibu Waziri - Sumeilam Jafo. Naibu.
Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Raisi, Muungano na Mazingira
  • Waziri - January Makamba
  • Naibu Waziri – Luhaga Jerrson Mpina
Ofisi ya Waziri Mkuu: Sera, Bunge, Kazi Vijana, Ajira na Walemavu
  • Waziri - Jenista Muhagama
  • MaNaibu – Dkt. Possy Abdallah na Anthony Mavunde.
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
  • Waziri - Mwigulu Nchemba
  • Naibu Waziri - William Ole Nasha
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
  • Waziri Bado hajapatikana.
  • Naibu Waziri – Inj. Edwin Ambandusi Ngonyani
Wizara ya Fedha na Mipango
  • Waziri Bado hajapatikana.
  • Naibu Waziri - Ashantu Kizachi
Wizara ya Nishati na Madini
  • Waziri - Prof. Mwigalumi Muhongo.
  • Naibu Waziri - Medalled Karemaligo.
Wizara ya Katiba na Sheria
  • Waziri - Harrison Mwakyembe
Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
  • Waziri - Dk. Augustino Mahiga
  • Naibu Waziri – Dkt. Susan Kolimba.
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
  • Waziri - Dk. Hussein Mwinyi
Wizara ya Mambo ya Ndani
  • Waziri - Charles Kitwanga.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
  • Waziri - William Lukuvi
  • Naibu Waziri - Angelina Mabula
Wizara ya Maliasili na Utalii
  • Waziri Bado hajapatikana.
  • Naibu Waziri– Inj. Ramol Makani
Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
  • Waziri Charles Mwijage.
Wizara ya Elimu,Sayansi Teknolojia na Ufundi.
  • Waziri Bado hajapatikana.
  • Naibu Waziri – Inj. Stella Manyanya
Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
  • Waziri - Ummy Mwalim
  • Naibu Waziri – Dkt. Hamis Kigwangala
Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo
  • Waziri - Nape Nnauye
  • Naibu Waziri - Anastasia Wambura.
Wizara ya Maji na Umwagiliaji
  • Waziri – Prof. Makame Mbarawa
  • Naibu Waziri– Inj. Isack Kamwela 

Mh.Rais John Pombe Magufuli katika picha ya pamoja na wanahabari waliofika kumsikiliza wakati akitangaza baraza la mawaziri Ikulu jijini Dar es salaam. Makamu wa rais Samia Suluhu Hassan na kushoto ni Waziri Mkuu Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa.

Wednesday, December 9, 2015

MH, RAIS JOHN MAGUFULI AFANYA USAFI UFUKWE WA FERRY.





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John P. Magufuli akiwa pamoja na Mke wake Mama Janeth Magufu katika  eneo la ufukwe wa ferry jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizoa taka katika  eneo la ufukwe wa ferry jijini Dar es Salaam.

Thursday, December 3, 2015

MH.RAIS MAGUFULI NA VIONGOZI WA UMOJA WA SEKTA BINAFSI.


Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli amewapa siku saba kuanzia tarehe 03/12/2015 wafanyabiashara wote ambao waliingiza mizigo yao bila kulipa kodi wakalipe kwani baada ya hapo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Hayo yamesemwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam na Mheshimiwa Rais katika mkutano wake na wadau wa sekta binafsi alipoamua kufanya mazungumzo nao pamoja na kuwasikiliza maoni yao ikiwa ni sehemu ya ahadi zake katika kipindi cha kampeni za kuomba kura za kiti cha Urais,lengo likiwa ni kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta binafsi.

Mheshimiwa Rais aliendelea kusema kuwa katika kipindi hichi cha miaka mitano amedhamiria kuijenga nchi na watu wasimuelewe vibaya kwa maamuzi anayofanya kwani ni kwania njema ya kuleta maendeleo na siyo ujeuri.

“Tutaangalia namna ya kupunguza utitiri wa ushuru katika bidhaa mbalimbali,mfano katika kipindi cha kampeni niligundua katika Mkoa wa Kagera na Kilimanjaro wanakolima zao la Kahawa,wamekuwa wakitozwa tozo 26 kwa zao hilo na hiyo imechangia kusababisha wafanyabiashara wa zao hilo kufanya biashara haramu ya kupeleka zao hilo kwa magendo kuuza katika nchi jirani”,alisema Mheshiwa Rais Dkt. Magufuli.

Pamoja na hayo Mheshimiwa Dkt.Magufuli amewaahidi wadau wasekta binafsi ushirikiano mkubwa kwani anatambua mchango wao katika kukuza uchumi na pia amewataka wadau hao kuwa wazalendo na kuliacha kukwepa kulipa kodi ili tuweze kujenga taifa lenye maendeleo makubwa ya kiuchumi.

Mheshimiwa Rais Dkt.Magufuli ameendelea kusema kuwa kama kutakuwa na mfayabiashara yeyote atakayetaka kuwekeza na akakwamishwa na mtu aliyechini ya uteuzi wake basi mtu huyo ataondoka kwani sasa ni wakati wa wadau wa sekta binafsi kuanza kuanzisha viwanda mbalimbali vitakavyo toa ajira.

Pamoja na hayo Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli amewapa mawazo ya kibiashara wadau wa sekta binafsi kuanzisha kampuni ya kutenganisha udongo unaotoka kwenye machimbo ya madini,kuanzisha viwanda vya samaki pembezoni mwa bahari pamoja na kutengeneza samani zitokanazo na mazao ya misitu.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw.Regnald Mengi amesema kuwa wako tayari kumpa ushirikiano mkubwa Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha uchumi watanzania unakuwa kwa haraka na pia amemuomba mheshimiwa rais kuendelea kukemea masuala ya rushwa pamoja kusaidia kupunguza utitiri wa kodi.

HOTUBA YA RAIS DK.JOHN P. MAGUFULI



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh, Dk. John Pombe Magufuli akiongea na Viongozi na Wawakilishi wa Umoja wa Sekta Binafsi nchini.

ZIARA YA KUSHTUKIZA BANDARINI NA TRL ALIYOIFANYA MH. MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimwonyesha Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es salaam, Bw. Abel Mhanga orodha ya makontena 2,431 yaliyopitia kwenye banda ya Dar es salaam bila kulipiwa kodi bandarini Desemba 3, 2015.

*Akuta makontena 2,431 yametoka bila kulipiwa ushuru
*Ataka majina yaletwe ofisini leo saa 11 jioni
*Atoa wiki wiki moja kwa mfumo wa malipo kubadilishwa
*Akagua mabehewa, awaweka kiporo TRL

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara nyingine ya kushtukiza bandarini na kukagua mfumo wa upokeaji na utoaji mizigo na utozaji wa malipo baada ya kupewa taarifa kwamba kuna makontena 2,431 yametolewa bila kulipiwa ushuru.

Waziri Mkuu alisema kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi wa bandari ya kuanzia Machi hadi Septemba 2014, makontena hayo yalipita bila kulipiwa kodi kupitia bandari kavu nne (ICDs) ambazo ni JEFAG, DICD, PMM na AZAM.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni watumishi 10 tu ambao wamesimamishwa kazi kutokana na makosa hayo. “Mmeamua kuwasimamisha kazi watu wadogo na kuwaacha wakubwa wanaendelea na kazi. Hatuwezi kuendelea kuikosesha Serikali mapato namna hii,” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amemtaka Kaimu Meneja wa Bandari, Bw. Hebel Mhanga amletee ofisini majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji kodi huo ifikapo leo saa 11 jioni. Pia amempa Meneja huyo wiki moja kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji malipo kutoka kwenye billing system na badala yake kuweka mfumo wa malipo wa kielektroniki (e-payment).

Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Desemba 3, 2015), wakati akikagua idara mbalimbali za mamlaka ya bandari na kuona ukaguzi wa mizigo unavyofanyika kwa kutumia scanners. Akiwa kwenye chumba cha scanner mojawapo, Waziri Mkuu alikuta manifest moja ikisema kontena limejaa diapers lakini picha ya kwenye kompyuta ya scanner ilionyesha kuwa ndani ya kontena hilo kuna vitu kama vifaa vya umeme.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja Bandari upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Ben Usaje ambaye pia ni msimamizi wa kitengo cha scanner, inapobainika taarifa kama hiyo inapaswa itumwe kwa wenye ICDs ili wafanye ukaguzi kwa kulifungua kontena ili kuhakikisha mali zilizomo ndizo zilizoandikishwa kwenye manifest.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amefanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za Shirika la Reli (TRL) na kukagua mabehewa yaliyokuwepo kisha akazungumza na baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo kwenye stesheni hiyo ambako alibaini madudu kwenye malipo ya mishahara na makato ya michango ya wafanyakazi.

Akizungumza na Mkurugenzi Mkuu TRL, Mhandisi Elias Mshana, Waziri Mkuu alisema amefika kwenye shirika hilo ili kujifunza utendaji wao kazi lakini anazo taarifa za wao kupewa fedha na Serikali kiasi cha sh. bilioni 13.5/- ili waendeleze miundombinu ya reli lakini hawakufanya hivyo. “Nia ya kuwapa fedha hizo ilikuwa ni kuboresha miradi ili muweze kujiendesha kibiashara lakini nyie mkaamua kujilipa wenyewe,” alisema.

“Ninazo taarifa kuwa baada ya hapo, mlikopa sh. bilioni 3 kutoka benki ya TIB ili kuendesha miradi ya shirika lakini badala ya kufanya miradi, fedha hizo mkaamua nazo kujilipa mishahara. Sasa sijui mnarudishaje huo mkopo wakati hakuna mradi wowote uliofanyika,” alihoji bila kupata majibu.

Alipoulizwa wafanyakazi wana matatizo gani hapo TRL, Katibu wa TRAWU, Bw. Boaz Nyakeke alisema wanadai malimbikizo ya makato yao kwenye mifuko ya pensheni, malimbikizo ya makato kwenye SACCOS na malimbikizo ya kuanzia Julai – Novemba 2014.

Waziri Mkuu kwa upande wake alimtaka Mhandisi Mshana asimamie uboreshaji huduma za usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam ili hata mabasi ya mwendo kasi yatakapoanza wananchi waweze kuwa na uhuru wa kuchagua aina ya usafiri wautakao.

“Tunataka kujenga yadi kubwa nje ya mji ili watu wenye magari wawe wanayaacha huko na kutumia usafiri wa treni au DART kuja mjini kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
ALHAMISI, DESEMBA 3, 2015.

Mh.Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu utoaji bili za kulipia kodi za serikali kwa watumiaji wa bandari ya Dar es salaam kutoka kwa ofisa mwandamizi wa masuala ya fedha, Bw. Sartho Mbuya wakati alipotembelea bandari hiyo Desemba 3, 2015 kutaka kujua ukweli wa tuhuma za makontena 2,431 yaliyopita bandarini hapo bila kulipiwa kodi za serikali.
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akitembelea stesheni ya reli ya Dar es Salaam Desemba 3, 2015.